Monday, August 11, 2014
0

Nchini Kenya wanaume kutoka kabila la Turkana na makabila mengine ambayo hayana utamaduni wa kuwapasha wanaume tohara wanaishi kwa hofu baada ya baadhi yao kutahiriwa kwa lazima na kundi la vijana kutoka kabila la Bukusu ambao kwa sasa wanaendelea na sherehe za kitamaduni za kuwapasha wavulana tohara.
Vijana hao wamekuwa wakiwavamia wanaume ambao hawajapitia kisu cha ngariba kutoka makabila mengine katika mji wa Moi’s Bridge Magharibi mwa Kenya na kisha kuwavua nguo hadharani, kuwapaka matope na maji taka kabla ya kuwapasha tohara kando kando ya barabara hata bila kudungwa sindano ya kutuliza maumivu.
Watu wa kabila la Bukusu huwachukulia wanaume ambao hawajakutana na kisu cha ngariba kuwa wachafu na waoga.
Lakini wanaume walioathirika wanalalamika kuwa Wabukusu wanawashurutisha kufwata utamaduni ambao sio wao.
Kumekuwa na ripoti za kuhitilafiana kwenye vyombo vya habari nchini Kenya kuhusu idadi kamili ya wanaume waliopashwa tohara kwa lazima, Mwandishi wa BBC Odeo Sirari alikutana na takriban wanaume 8 ambao waliopashwa tohara kwa lazima.
Baadhi ya wanaume hao walisema kuwa walikuwa na bahati ya kupelekwa kwa lazima hadi kituo kimoja cha afya katika mji huo na kisha kupashwa tohara katika mazingira safi.
Lakini Paul Korobei hakuwa na bahati kama hiyo.
Watu wa Jamii ya waturkana waliolazimishwa kupashwa tohara
Nilimkuta kitandani akiwa na uchungu katika chumba chake kidogo nje kidogo ya mji huo wa Moi’s Bridge.
Alipashwa tohara kwa lazima kandokando ya barabara.
‘’ Nilikuwa njiani kuelekea mjini kwa shughuli zangu za kuuza karanga ndipo nikavamiwa na kundi la vijana.
Walinipokonya baiskeli yangu na kisha kunipasha tohara kwa lazima.’’ Anasema Korobei.
‘’ Singeweza kuendelea na shughuli zangu kutokana na kilichotendeka.
Sikuwa na budi ila kurudi nyumbani kuuguza majeraha yangu.
Ilipopambauka, polisi walikuja na kunichukua hadi hosipitalini.
Sikupata matibabu ya kutosha-walinifunga tu bendeji na kuniacha hivyo.
Dawa unaozoona hapa, nilinunua mwenyewe.’’ Anasema bwana Korobei.
Maisha yake yamekwama kutokana na majeraha aliyopata.
Bwana Loktutuk ambaye anakwepa tohara ya lazima
Hawezi kuendelea na shughuli yake ya kuuza njugu karanga kutokana na maumivu, ilhali ana mke na watoto wanaomtegemea.
Wanaume kadhaa wa kabila la Kiturkana katika mji huu sasa wanaishi kwa hofu na baadhi yao wamekwenda mafichoni ili kuepuka kisu cha ngariba.
Peter Loituktuk amekuwa akilala kichakani kwa sababu majirani wake ni wa kabila la Bukusu na ana wasi wasi kwamba huenda wakamsaliti.
‘’Hebu nitazame.
Niko mbioni kwa sasa. Nimejitokeza tu baada ya kusikia kwamba maafisa wa serikali wamekuja kutusaidia.
Jambo hili halipaswi kutokea. Mke wangu ni mjamzito, ikiwa nitapashwa tohara kwa lazima, ni nani atakayemtunza yeye na mtoto atakayezaliwa?’’ Akashangaa Loktuktuk.
Wengi wa vijana wanaotekeleza unyama huu wametoweka na wachache waliotambuliwa walikataa kuzungumza wakihofu kukamatwa na polisi.
Nilienda katika mji jirani wa Kamukuywa ambapo sherehe ya kuwapasha wavulana tohara ilikuwa ikiendelea.
Niliwauliza baadhi ya watu maoni yao kuhusu hatua ya wenzao katika mji wa Moi’s Bridge kuwapasha tohara wanaume kutoka makabila mengine.
‘’ Sisi hatulazimishi mtu yeyote kupashwa tohara. Ikiwa wanafanya hivyo kule basi ni makosa.’’ Alisema Martin Makongwe.
Wavulana wanaosubiri kupashwa tohara alfajiri wanaendelea kuimba nyimbo za kuwatia mori katika kijiji cha Nakalira.
‘’ Hili ni tukio lenye umuhimu mkubwa kwa jamii ya Wabukusu.
Ni wakati ambapo wavulana wetu huvua nguo( ana maana ngozi ya uume) waliozaliwa kutoka tumbo la mama na kuwa watu wazima,’’ anasema Wamukota Ndombi.
Polisi katika mji wa Moi’s Bridge walikata kujjibu shutuma kwa kwamba hawakuchukuwa hatua kwa haraka kuwaokoa wanaume hao.
Kamanda wa kituo cha polisi cha Moi’s Bridge alisema kuwa haruhusiwa kuzungumza na vyombo vya habari.
Lakini chifu wa eneo hilo Bwana Wilson Sirma alisema kisa hicho nusura kizue uhasama wa kikabila katika eneo hilo ambalo lilifanikiwa kuepuka machafuko ya kikabila yaliyotokea nchini Kenya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.
‘’ Ni kweli polisi walishindwa kuchukua hatua kwa dharura.
Hata hivyo niliweza kutumia maafisa wangu kudhibiti hali.
Jumla ya wanaume sita walitahiriwa kwa lazima.’’ Alisema bwana Sirma.

0 comments:

Post a Comment

MAONI YAKO HAPA

Name

Email *

Message *

MARAFIKI

WANAO NITEMBELEA