 |
Rais Dk.Jakaya M. Kikwete akiwa na Askofu Dk.Alex Malasusa, (picha na library..), salamu za maasakofu wa KKKT, ni hizi hapa chini...... |
|
|
|
|
Waumini wa KKKT, Wakristo Wote na Watanzania kwa Ujumla.
Neema na Iwe kwenu na
amani itokayo kwa Mungu Baba na Bwana wetu Yesu Kristo, Amina.
Sisi maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT), tumepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za matukio ya uchomaji wa makanisa
katika eneo hili la Mbagala. Tumekuwa katika mkutano wetu wa Mwaka wa Lutheran
Mission Cooperation (LMC) huko Moshi pamoja na vyama vyote vya Kimissioni vya
Ulaya na Marekani. Tumelazimika kukatisha mkutano huo ili kufika hapa Mbagala.
Tumekuja kwa madhumuni makubwa matatu:
1.
Tumekuja kuwapa pole
na kusimama pamoja nanyi katika uchungu mkubwa mlio nao. Machozi yenu ni
machozi yetu. Machozi yetu ni machozi ya Kristo mwenyewe aliye Bwana wa kanisa
linaloteswa. Jipeni moyo kwa kuwa yeye aliushinda ulimwengu (Yohana 16:33).
2.
Tumekuja kuonyesha
majonzi yetu makubwa kwa vitendo vya uvunjifu wa amani, kuporomoka kwa umoja na
mshikamano wa watanzania. Huu ni msiba mkubwa, na wenye msiba ni watanzania
wote, wenye dini na wasio na dini.
3.
Tumekuja kushiriki
pamoja nanyi kupokea matumaini ya Tanzania mpya. Katika majivu haya
yaliyotokana na kuchomwa kwa madhabahu ya Mbagala, Tanzania mpya itazaliwa.
Majivu haya na machozi yenu ni rutuba ya Tanzania mpya itakayojali upendo,
uvumilivu, ustahimilivu, umoja, mshikamano, uhuru wa kuabudu na dola isiyo na
dini.
Katika ujio huu wa maaskofu hapa Mbagala, hatukuja hapa kufanya
haya yafuatayo:
1.
Hatukuja kuwahukumu
hata kama hatukubaliani na wanaokashifu dini za wenzao, wawe na ruhusa kutoka
mamlaka zilizo juu au kama wanajituma wenyewe.
2.
Hatukuja kuwahukumu
hata kama hatukubaliani na wanaodhalilisha misahafu ya dini; wawe wametumwa,
kutegeshewa na mamlaka zozote au kwa misukumo ya utashi wao binafsi ili kupata
kisingizo cha kugombanisha madhehebu ya dini.
3.
Hatukuja kuwahukumu
hata kama hatukubaliani na wanaochoma makanisa na kuiba mali za makanisa kwa
kisingizio cha kumtetea Mungu. Kisasi cha dhambi hiyo tunamwachia Mungu
mwenyewe aliyedhihakiwa na walionajisi madhabahu yake.
Wapendwa wana KKKT na watukuka sana, wana na mabinti wa Tanzania
ya Julius Kambarage Nyerere; kilichotokea Mbagala katika wiki ya kuadhimisha
siku ya Baba wa Taifa, ni kebehi si kwa Baba wa Taifa bali ni kebehi kwetu sisi
wenyewe tunaokalia kiti alichokalia Baba wa Taifa. Yeye amelala baada ya kazi
njema. Apumzike kwa amani na tunu zake zifufuke katika majivu haya yaliyotokana
na kuchomwa kwa amani na mshikamano wa Tanzania aliyoijenga.
Kilichotokea Mbagala
ni mateso ya kimbari, yaani mateso ya Kanisa (Persecution). Mateso haya ni
matokeo ya mbegu ya magugu iliyopandwa katika bustani njema na sasa magugu hayo
yanazaa matunda machungu. Dalili za mateso ya kimbari kama ilivyo kwa mateso ya
kanisa; zilianza kitambo na hazikushughulikiwa na waliomrithi Baba wa Taifa.
Dalili hizo ni kama hizi zifuatazo:
·
Uchochezi wa wazi kuwa
taifa hili linaendeshwa na unaoitwa “mfumo Kristo”, na kuwa Baba wa Taifa
alaaniwe kwa yote aliyolitendea taifa hili.
·
Ubishi usio na tija
juu ya idadi ya waumini wa dini mbalimbali hapa nchini na hata kudiriki
kushawishi na kugomea zoezi la sensa ya watanzania. Lengo la ubishi huu ni
mbegu inayoweza kuratibisha na kurasmisha mateso ya kimbari na mateso ya
kanisa.
·
Matumizi mabaya ya
baadhi vyombo vya habari, vyenye lengo la kujenga hofu ya kudumu na migawanyiko
ya kidini miongoni mwa watanzania
·
Ukimya wa vyombo vya
dola juu ya vitendo vya uvunjaji wa sheria ya matumizi ya vyombo vya habari. Kwa
vyovyote vile, uvumilivu wa dola hauna maslahi mapana kwa mustakabali wa taifa
letu na ni mateso ya kimbari, mateso kwa kanisa, na kwa wantanzania wote; wawe
wengi dhidi ya wachache au wachache dhidi ya wengi.
·
Madai yasiyo ya
kawaida na ya mara kwa mara kwa serikali inayodaiwa kutokuwa na dini. Madai
hayo ni kama:
1.
Kulazimisha uvaaji wa
alama za kidini katika taasisi za umma ili kurahisisha na kuratibisha tofauti
za watanzania. Tunajiuliza: Likitokea la Mbagala katika mashule yetu na vyuo
vya umma, watachomwa wangapi na kuuawa wangapi?
2.
Madai
yanayojirudiarudia kutaka balozi za nchi fulani kufungwa hapa nchini. Madai
haya yanaashiria kutaka balozi za nchi fulani tu ndiyo ziwe hapa nchini.
3.
Madai na mashinikizo
ya Uanzishwaji wa mahakama za kidini hapa nchini
4.
Mashinikizo ya kidini
yanayoingilia mifumo ya kitaaluma na kisheria.
5.
Mashinikizo ya kidini
juu ya mfumo wa uteuzi wa watendaji wa serikali na katika ofisi za umma,
6.
Kuhoji na kupotosha
juu ya ushirikiano wa serikali na mashirika ya dini katika utoaji wa huduma za
kijamii hususan afya na elimu hapa nchini
Wapendwa wana KKKT na Wapendwa watanzania wote. Hata kama
wanaofanya mambo haya ya kusikitisha wametunukiwa hadhi ya kuitwa kuwa ni “wana
harakati”, tofauti na wanaharakati wanaotambuliwa na watanzania walio wengi,
tunawiwa kuonya kwa uvumilivu wote kuwa uana harakati wao usitumike kuvunja
nchi na sheria za nchi. Tanzania yenye amani na mshikamano ni tunda la dini
zote, makabila yote, itikadi zote za vyama, rangi zote na hali zote za
kiuchumi. Hata wasio na dini wanachangia amani ya nchi hii.
Kwa macho na masikio
yetu, tumeendelea kushuhudia vitendo vya uchomaji makanisa huko Zanzibar,
Mwanza, Mdaula, Mto wa Mbu, Tunduru, Rufiji, Kigoma na sasa Mbagala. Wakati
wote uvumilivu wa wakristo huenda umetafsiriwa kuwa ni unyonge na woga.
Ikumbukwe kuwa hata wanyonge na waoga, hufika wakati wakasema “sasa basi” pale
wanapodhalilishwa kupita kiasi. Hatuombei wakristo wafikishwe hapo.
Tumeshuhudia wizara
zetu zikivamiwa mchana kweupe na kushinikiza kuachiwa kwa watuhumiwa wa
uhalifu; tumeshuhudia vituo vya polisi vikichomwa moto; mahakama zikilazimishwa
kufunga shughuli zake, misikiti ikitekwa, uhai wa viongozi wa dini ukitishiwa
hadharani na viongozi wastaafu wakizabwa vibao hadharani kwa sababu ya
zinazoitwa harakati za kidini. Tumefikia kuhoji, watu hawa wavamie nini ndipo
hatua zichukuliwe? Wachome nini ndipo viongozi wenye dhamana ya kulinda mali na
uhai washtuke? Wamwue nani ndipo iaminike kuwa watu hawa ni tishio kwa usalama
wa taifa letu?
Sisi tulioitwa kwa
njia ya nadhiri na viapo vitakatifu, tunawasihi sana waumini wa dini zetu na
watanzania kwa ujumla, wenye wajibu wa kututii na wasiolazimika kututii,
kuzingatia kuwa Mwenyezi Mungu analipenda taifa hili na watu wake. Kamwe hawezi
kuliacha liangamie.
Kwa Wakristo wote, huu
ni wakati wa kuendelea kufunga na kuomba kwa ajili ya amani ya taifa hili.
Mkristo wa kweli ni yule aliye tayari kuteswa kwa ajili ya Kristo na kanisa.
Wakristo hatuko tayari kuua, kutesa, kulipiza kisasi ili kumtetea Kristo. Mungu
wetu hatetewi kwa kuua wengine na kuchoma madhabahu ya dini nyingine.
Katika mateso haya,
kanisa litaimarika zaidi; na katika majivu haya ya Mbagala, Tanzania mpya
itazaliwa na ukombozi wa kweli utapatikana. Tunawataka wakiristo wote kusamehe
na kuendelea kuwa raia wema. Kushiriki kikamilifu katika kuleta mabadiliko ya
kweli kwa kupitia njia sahihi zilizowekwa. Wakati wengine wanaweka mikakati ya
kuchoma madhabahu, wakiristo tuweke mikakati ya kuomba na kushiriki vema katika
haki zetu za uraia. Pamoja na kuwa wapole kama njiwa, imetupasa pia kuwa na
busara kama nyoka (Mathayo 10:16).
Daima tukumbuke
kuwa, “KUSHINDANA KWETU SISI SI JUU YA DAMU NA NYAMA BALI NI JUU YA
FALME NA MAMLAKA, JUU YA WAKUU WA GIZA HILI, JUU YA MAJESHI YA PEPO WABAYA
KATIKA ULIMWENGU WA ROHO” (Waefeso 6: 12).
Ni sisi Maaskofu wenu kwa Neema ya Mungu,
1.
Askofu Dr. Alex G.
Malasusa – Mkuu, KKKT na D/Mashariki na Pwani
2.
Askofu Dr. Stephen
Munga –Mkuu, D/Kaskazini Mashariki
3.
Askofu Dr. Martin Shao
– Mkuu, D/Kaskazini
4.
Askofu Dr. Thomas
Laizer – Mkuu- D/Kaskazini Kati
5.
Askofu Dr. Benson
Bagonza- Mkuu, D/Karagwe
6.
Askofu Isaya J.
Mengele – Mkuu, D/Kusini
7.
Askofu Levis Sanga –
Mkuu- D/Kusini Kati
8.
Askofu Elisa Buberwa –
Mkuu –D/Kaskazini Magharibi
9.
Askofu Andrew Gulle –
Mkuu, D/Mashariki ya Ziwa Victoria
10.
Askofu Michael Adam
–Mkuu, D/Mkoani Mara
11.
Askofu Renard Mtenji –
Mkuu, D/Ulanga-Kilombero
12.
Askofu Dr.
Israel-Peter Mwakyolile – Mkuu, D/Konde
13.
Askofu Job Mbwilo –
Mkuu, D/Kusini Magharibi
14.
Askofu Dr. Owdenburg
Mdegella- Mkuu, D/Iringa
15.
Askofu Jacob Ole
Mameo- Mkuu, D/Morogoro
16.
Askofu Zebedayo Daudi
– Mkuu, D/Mbulu
17.
Askofu Paulo Akyoo –
Mkuu, D/Meru
18.
Askofu Charles Mjema –
Mkuu, D/Pare
19.
Askofu Mteule Amon
Kinyunyu- Mkuu, D/Dodoma
20.
Askofu Mteule Dr. Alex
Mkumbo- Mkuu, D/Kati
Mbagala, Dar es
Salaam,
Oktoba 18, 2012
0 comments:
Post a Comment
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.